Monday, April 9, 2007

Utalii Ukiwezeshwa Tutaendelea
Na Aisha Mbaga
SERIKALI inaposhauriwa katika mabo yanayoendeleza nchi, nivyema ikatilia mkazo kwani wakati mwingine huwa ushauri unafaida kwa taifa,
kama tunakumbuka kipindi cha uongozi wa serikali ya Dk Salmin Amou, alitoa uamuzi wa kuruhusu sekta ya utalii Visiwani iendelezwe lakini mwanzoni uamuzi huo ukipingwa na wengi ikiwa ni pamoja na kulalamikiwa na baadhi ya wananchi ambao hawakuwa wakielewa vyema matokeo yake.
Kwa sasa wananchi wengi wanaona faida ya uamuzi huo na wengi wameuunga mkono kutokana na sekta hiyo kuleta matunda kwa wananchi wa Zanzibar na serikali kwa ujumla .
Rais Mstaafu Dk Salmin Amour na serikali yake walifikia uamuzi wa kuruhusu sekta ya utalii kuchipua mwaka 1992 kama njia ya kuongeza vyanzo vya mapato na kuinua hali za maisha ya wananchi wake.
Kutokana na umuhimu wa sekta hiyo, mwaka 1996, Dk Salmin aliamua kuanzisha kamisheni ya Utalii na kutunga sheria No. 9 ya mwaka 1996 ambayo inasimamia sekta hiyo.
Uamuzi huo, uliwashtua watu wengi na kupata upinzani wa chini kwa chini kwa vile faida zake zilikuwa hazionekani wakati huo.
Hatua hiyo, ilisababishwa na wasiwasi wa baadhi ya wananchi kuwa suala hilo linahusu mila na utamaduni, na kuhofia kuathirika kwa utamaduni wa Mzanzibari.
Hata hivyo malengo ya Dk. Salmin yalionekana tofauti na mawazo yao, kwa vile sekta hiyo hivi sasa imeleta faida kubwa kwa serikali na wananchi wake baada ya bei ya zao la karafuu kuporomoka katika soko la dunia.
Zao la karafuu lilitegemewa sana katika kuchangia pato la taifa tangu utawala wa kifalme wa Sultani na baada ya mapinduzi ya Zanzibar kwa vile mzunguko mkubwa wa fedha kwa wananchi wake ulitegemea zao hilo.
Mwenyeketi wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZTC) Issa Ahmed Othman anasema sekta ya utalii Zanzibar kwa sasa inachangia asilimia 20 ya pato la taifa kutokana na watalii wanaotembelea Zanzibar kutoka nchi mbalimbali duniani hasa Ulaya.
Anasema kuwa kuanzia mwezi wa Julai hadi Desemba mwaka jana, watalii wapatao 135,000 walitembelea Zanzibar, kiwango ambacho ni kikubwa kulinganishwa na watalii 125,443 waliotembea Zanzibar kipindi kama hicho mwaka 2005.
Alisema katika kipindi cha Januari pekee mwaka huu, watalii 14,117 walitembelea Zanzibar, kiwango ambacho hakijawahi kutokea katika kipindi cha mwezi mmoja kutembelewa na idadi kubwa ya watalii kama hiyo.
Mwenyekiti alisema kuwa, zipo sababu tatu za kuimarika sekta ya utalii Zanzibar, ikiwemo kwamba Zanzibar haina majanga ya kutisha, utulivu wa kisiasa, pamoja na kuwa na maeneo mengi yanayowavutia watalii.
Hata hivyo alisema, sekta hiyo inakabiliwa na matatizo makubwa mawili, kukosekana kwa watu wenye taaluma ya juu katika sekta ya utalii, kukosekana kwa soko la vyakula na matunda na hivyo kulazimika kutegemea kutoka nje ya Zanzibar.
``Sekta ya utalii ina tatizo la ukosefu wa watu wenye taaluma ya utalii na kulazimika nafasi nyingi kushikwa na watu kutoka nje ya Zanzibar,`` Akasema Mwenyekiti huyo.
Alisema kuwa, wakati Chuo cha Utalii Zanzibar- Maruhubi, kinatoa wanafunzi wenye kiwango cha cheti, uwekezaji wa utalii Zanzibar unakua na unahitaji watu wenye taaluma ya stashahada na shahada ya Chuo Kikuu.
Aidha alisema kwamba kumefika wakati Zanzibar iwe na shirika lake la ndege, kwa vile ina uwezo wa kulitumia soko hilo kwa watali wanao safari kati ya Zanzibar na mataifa ya Ulaya na Tanzania Bara.
``Watalii wanaosafiri kati ya Zanzibar na mikoa ya Tanzania Bara kuangalia vivutio vya utalii, bado hawana uhakika wa usafiri wa anga kwa vile ndege zinazotumika ni ndogo,`` Anasema Mwenyekiti.
Alisema kuwa, ni kweli Zanzibar ina mchango wake katika Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) lakini tangu shirika hilo kubinafsishwa, na Serikali ya Muungano, limeimarisha zaidi safari zake kati ya Tanzania na Afrika Kusini wakati watalii wanatembelea Zanzibar wanatoka nchi za Magharibi na Ulaya.
Alisema kwamba, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, sekta ya utalii Zanzibar inahitaji kuimarishwa katika sekta ya ulinzi ili kuwaondolea usumbufu watalii.
``Utaratibu wa kuwafanyia upekuzi watalii kwa kufungua mabegi yao na kuyapekua, umepitwa na wakati, lazima tuwe na vifaa vya kisasa ili tusiwapotezee muda wao wanapopita uwanja wa ndege,`` alisema Bw Othman.
Hata hivyo alisema ni kweli unapowakawiza wawekezaji, kuna faida na hasara lakini la msingi ni kuendelea kuheshimu mila na utamaduni.
``Unapokaribisha uwekezaji, ni sawa na kufungua dirisha, kila mdudu ataingia wakiwemo mbu na inzi. Cha msingi ni kuheshimu mila na utamaduni kama kweli tunataka kuwa na jamii bora `` Anasema Mwenyekiti huyo.
Akasema kwamba jambo la msingi lazima wanaume wakubali kubadili tabia, kwa vile wao ndio wanaoimarisha biashara ya ukahaba, na sio haki kuwachukulia hatua wanawake wanaojiuza kwa kutumia vibaya sekta ya utalii.
Aidha anasema kwamba, sekta ya utalii hadi hivi sasa inahitaji kuwa na mfumo mpya wa ukusanyaji mapato kutoka katika sekta hiyo ili takwimu sahihi ziwe zinapatikana.
Akasema kuwa hivi sasa vyombo ni vingi vinavyokusanya mapato, ikiwemo Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Baraza la Manispaa, Halmashauri za Wilaya, pamoja na jumuiya zisizokuwa za serikali zinazojishughulisha na sekta hiyo.
Anasema kwamba, sera ya utalii iliyopitishwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, itafanikiwa kama taasisi zote za serikali zitaamuwa kuimarisha sekta za miundo mbinu, kilimo na uvuvi, ili Zanzibar iondoke katika kutegemea bidhaa za vyakula kutoka Tanzania bara katika soko hilo.
Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar, Bw Mohamed Ismail anasema kwamba wameamua kufanya ukaguzi usiku katika mahoteli ya kitalii baada ya kujitokeza vitendo vya udangayifu kwa wawekezaji.
Akasema kwamba maafisa wa bodi hiyo, wamekuwa wakifanya kazi saa 24, ikiwemo kukagua vyumba vya hoteli ambavyo havina wageni ili kuweka kumbukumbu sahihi za ulipaji kodi.
``Kuna baadhi ya wafanyabiashara, walikuwa wanapokea wageni 200 kwa siku, lakini wanalipia kiwango kidogo cha wageni, na utaratibu huu wa kufanya ukaguzi umetusaidia sana,`` Akasema kamishna Ismail.
Akasema kwamba, ukusanyaji wa mapato Zanzibar umeongezeka kwa asilimia 105.4 kutoka mwaka 1999 hadi mwaka wa fedha wa 2005/2006.
Akasema katika mwaka huu wa fedha bodi hiyo inatarajia kukusanya sh bilioni 60 kutoka sh bilioni 44.3 ambapo kila mwezi wanatarajiwa kukusanya sh bilioni tano badala ya sh bilioni 3.5.
Alisema kwamba, fedha hizo zinatoka katika vyanzo vitatu vya mapato ikiwemo sekta ya Utalii,mafuta na biashara.
Hata hivyo, baadhi ya wananchiZanzibar,wanasema sekta ya utalii Zanzibar imeyumbisha mila na utamaduni wa Mzanzibari kwa vile mavazi mengi wanaovaa vijana wakiwemo wasichana hayana tofauti na wanayovaa watalii wanayotoka nchi za ulaya.
``Zanzibar haikuwa rahisi kumuona msichana kavaa nguo fupi kitovu wazi,au nywele wazi, lakini hivi sasa ni vitu vya kawaida , na tunaamini hali hii imechangiwa na utandawazi katika sekta ya utalii,``Akasema Bw Abdulrahman Saleh mkazi wa Mkunazini.
Sheikh Suleiman Masoud wa Mtaa wa Kiponda anasema kuwa pamoja na sekta ya utalii kutoa mchango mkubwa, bado serikali inapasa kuwaeleimisha watalii wanapofika Zanzibar kuvaa nguo za heshima wanapotembelea mitaa mbalimbali hasa mji mkongwe.
``Tunaifundisha jamii yetu nini, kama wageni wanapita mitaani huku nguo za ndani zikionekana?
Tusijaribu kuacha utamaduni wetu, bado muda wa kuwaelimisha wageni upo,`` Akasema Zainab Kombo mkazi wa Vuga.
Pamoja na kuimarika kwa sekta ya Utalii Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ),bado inahitajika kuimarisha Chuo cha Utalii kilichopo Marhubi, ili vijana waweze kunufaika na sekta badala ya kuajiri vijana kutoka nchi jirani za Kenya, na Uganda.
Aidha sheria ya kazi No 3 ya mwaka 1997,na marekebisho yake lazima isimamiwe vizuri na kamisheni ya kazi Zanzibar ili iweze kuwanufaisha wafanyakazi wazalendo, ambao wana tofauti za mishahara kwa asilimia zaidi ya 80 na wafanyakazi wenzao wageni.
Pamoja na sheria hiyo, kuwapa uwezo maafisa wa kamisheni ya kazi kuhakikisha mikataba ya kazi wanaikagua kabla ya kufikiwa, kati ya wawekezaji na wafanyakazi wa kizalendo,lakini mikataba isiyozingatia sheria imeendelea kuwa kero katika sekta hiyo.
Wafanyakazi wengi wa kizalendo, wamekuwa wakifungishwa mikataba ya muda mfupi na kushindwa kunufaika na sheria ya mfuko wa Hifadhi wa Jamii Zanzibar,(ZSSF),kutopatiwa posho ya likizo, nyumba, matibabu, pamoja na malipo ya kazi za ziada.
mwisho

No comments: