Saturday, March 31, 2007

Mrema amcharukia Tao kwa madai ya Mahakama

Na Aisha Mbaga

MWENYEKITI wa Chama Cha Tanzania Labour (TLP) Agustine Mrema, amesema amekanusha taarifa za kuwa amezuiwa na Mahakama Kuu kufanya shughuli za chama wala kutumia fedha kama inavyoelezwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Hamadi Tao.

Kauli hiyo ya Mrema, imetokana na taarifa ya Tao, ambayo ambayo amelieleza Tanzania Daima kwamba mahakama imetia uamuzi wa kumzuia Mrema asijiusishe na kazi za chama wala kutumia fedha za chama hicho.

Akizungumza kwa njia ya simu jana Mrema, alisema kuwa, yeye hajashindwa kesi na pia hajapewa barua ya kufungiwa kwa chama chake na kuzuiwa kuitisha kikao cha kamati kuu ya chama hicho.

Mrema alisema kuwa, yaliyopo mahakamani ni malalamiko na kila mtu ana uhuru wa kwenda Mahakamani kupeleka malalamiko yake na akasikilizwa hivyo Tao anahaki hiyo asubiri maamuzi ya Mahakama yatakaposikiliza lalamiko lake.

Pia alisema kuwa,TLP kwa sasa haimtambui Tao kuwa ni mwanachama wa chama hicho kwakuwa Kikao cha Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama hicho kilimfukuza uanachama yeye na wenzake 23 baada ya kubainika kuwa ni waasi wa chama hicho.

"Siwezi kuacha kuendelea na shughuli za chama changu kwa kuwa sijapewa barua ya kusimamisha shughuli na TLP bado haijavunjwa, pesa tunazotumia ni kwaajili ya shughuli za chama na katiba yetu inaturuhusu kutumia pesa za chama kwa shughuli za chama,"alisisitiza Mrema.

"Ndugu Mwandishi huyo Tao,kuwa nae makini kwakuwa ana kila dalili za kuchanganyikiwa akili kwakuwa ni yeye mwenyewe ndiye aliyeenda kufungua Mahakama Kuu,akipinga kufukuzwa uanachama, sasa mahakama bado haijatoa uamuzi.....yeye ameishaanza kupita kwenye vyombo vya habari kuwaletea habari za uongo ambazo msipokuwa makini naye mkazichapisha gazeti letu litaishia kushitakiwa kwaajili yake",alisema Mrema.

"Tao nakwambia usinifuate futae, mimi siyo saizi yako, tulia nyumbani kwako usubiri mahakama itatoa uamuzi gani kwenye kesi iliyofungua....kwanza kitendo hichi unacho kifanya ni kinyume na sheria kwakuwa mahakama bado haijatoa uamuzi wewe unapita kwenye vyombo vya habari kusema bahari za uongo ambazo mahakama haijazisema na sema hivi mchezo huo unaidharirisha mahakama yetu ambayo tunaimani nayo." alisema Mrema.

Hata hivyo Mrema aliviomba vyombo vyote vya habari kuwa makini na Tao, kwakuwa amekuwa akitoa taarifa za uongo kuhusu shauri lililopo mahakamani kuwa limeishatolewa uamuzi jambo ambalo si kweli.

Mrema alisema hawatishiki na kauli za Tao na kusema kuwa TLP itaendelea na shughuli za kichama kama kawaida kwakuwa ni moja ya haki za msingi ya chama hicho na kuongeza kuwa April 3,mwaka huu, chama chake kitafanya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa na Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF, Professa Ibrahim Lipumba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Mapema jana asubuhi aliyekuwa Katibu wa chama hicho Hamadi Tao, alitembelea ofisi za gazeti hili alisema Mahakama Kuu,imezuia vikao vya TLP hadi itakapotoa maamuzi lakini ameshangazwa na kitendo cha Mrema kuitisha kikao cha kamati kuu bila kuwashirikisha.

Tao alisema kuwa, kutokana na kufukuzwa uanachama wa TLP walifungua kesi Mahakama Kuu wakidai fidia ya Milioni tano na kutaka kusimamisha kwa shughuli zote za chama hadi Mrema kutokana na ubadhirifu wa fedha za chama hicho unaofanywa na Mrema kwa manufaa yake mwenyewe.

Alisema kuwa, pia wamefungua kesi nyingine katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakiomba kukaguliwa kwa mahesabu ya TLP na wakaguzi wa serikali ili kubainisha matumizi sahihi ya chama hicho.

Tao aliongeza kuwa, Katika kesi iliyopo Mahakama Kuu namba 138 ya mwaka 2006, wanaiomba Mahakama pia iwarudishie uongozi wao na kutambuliwa kama wanachama halali wa chama hicho na kesi ya Kisutu wanaiomba Mahakama isimamishe shughuli zote za chama hicho ikiwa ni pamoja na kuzuia matumizi ya fedha za chama hicho.

Mwisho.

No comments: