Friday, March 16, 2007

UHUMI WA TANZANIA UTABOREKA TUNa Aisha Mbaga
RAIS wa Jamuhuri ya Muungano Tanzania, Jakaya Kikwete, amesema serikali ya awamu ya nne itaendelea kuamini kuwa, sekta binafsi ni moyo wa uchumi na maendeleo ya Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Kikwete alisema kuwa, Serikali, imeweka mazingira mazuri katika kuhakikisha kuwa, fursa zote zilizopo kwenye uwekezaji, zinatumika kikamilifu kwa manufaa ya Taifa.
Hali kadhalika, alieleza kwamba, amewataka wawekezaji wa nje na ndani, kujenga imani na serikali yake ambayo alisema itafanya kazi na wadau hao kwa faida ya pande zote.
Katika Mkutano wa sita ulioandaliwa na Baraza la Taifa la Biashara(TNBC) uliofanyika mjini arusha, aliwataka wawekezaji kuwa na imani na Tanzania kwani ni nchi ambayo inaamani na inayopiga hatua kimaendeleo.
Lengo la mkutano huo ilikuwa n i kujadili masuala muhimu ya kiuchumi yatakayoiwezesha Tanzania kuondokana na mfumo wa uchumi hodhi.
Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa TNBC, alisema kwa kuthamini mchango unaotolewa na wawekezaji wa ndani na nje, serikali yake imekuwa ikifanya mabadiliko katika baadhi ya sheria za biashara, zilizoonekana kukwamisha mikakati ya kuwezesha wawekezaji wa nje kuja nchini kuwekeza, hususan wa sekta za viwanda, madini na kilimo.
Alitaja baadhi ya sheria ambazo zimekuwa changamoto kwa wawekezaji wa ndani na nje zilizofanyiwa marekebisho kuwa ni ya ardhi na sheria ya kazi ambayo wawekezaji wengi ama waajiri wengi, wamekuwa wakidai kwamba, zinawakandamiza mno waajiri na kuwapendelea zaidi waajiriwa.
Alisema Kikwete Kuwa, "Kwa kuthamini mchango wa wawekezaji ambao wamekuwa wakisaidia maendeleo ya taifa, hususani katika suala la mapato ya serikali kutokana na biashara wanazoziendesha, serikali imekuwa ikijiendesha kutokana na kodi zinazotozwa toka kwenye sekta binafsi",.
Alisema, tayari Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeaanza kuangalia sheria hizo.
Alitaja hatua nyingine ambayo serikali ipo kwenye mchakato wa kuifanyia marekebisho kuwa ni ya vibali na leseni za biashara hapa nchini, hususan kwa wawekezaji wa nje.
Alisema kupitia mkutano uliopita wa Baraza la Taifa la Wafanyabiashara, wawekezaji wa nje walieleza kwamba changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni vibali vya kufanyia biashara kuwa vya bei ghali ikiwa ni pamoja na urasimu wa kuvipata.
Rais Kikwete alisema, tayari ameziagiza mamlaka husika, kuangalia upya suala hilo ambapo alieleza kwamba, kiwango cha kulipia vibali vya kufanya biashara hapa nchini kitapunguzwa kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Aidha alisema, "azma ya serikali kwa kushirikiana na baraza hilo ni kuhakikisha sekta binafsi zinapewa nafasi ya kuongoza ujenzi wa uchumi wa nchi, huku serikali ikiwa na kazi moja ya kujenga mazingira bora zaidi ya ufanyaji biashara".
"Natumaini kupitia mkutano huu, kasi dhidi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa letu itaongezeka maradufu kupitia sekta binafsi zitakazowekeza hapa nchini, hasa kwa upande wa elimu, kilimo, utalii, viwanda, miundombinu, mawasiliano na sekta ya madini", alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo, aliwataka wawekezaji kushirikiana na serikali katika kuboresha miundombinu, hususan ya barabara, ambapo alisema wawekezaji nao ni muhimu wakachangia ujenzi wa barabara badala ya suala hilo kuachiwa serikali pekee.
Kutokana na mabadiliko ya utandawazi pamoja na kuongezeka kwa gharama za kuendeshea sekta ya utalii, Rais alisema kuwa serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ipo kwenye mpango wa kuongeza kodi ya watalii wanaoingia nchini kila mwaka kwa ajili ya kutembelea mbuga za wanyama.
Alisema gharama zimekuwa ni ghali mno kuliko awali hasa suala la kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo ya hifadhi za Taifa pamoja na barabara zinazokwenda kwenye hifadhi hizo.
"Serikali iko kwenye mchakato wa kuongeza kodi za watalii wanaoingia, ili kuboresha huduma ya utalii na kuongeza pato la Taifa", alisema JK.
Kuhusu suala la sekta ya kilimo, Rais Kikwete alisema kwa kuthamini kilimo ambacho ndicho uti wa mgongo wa taifa, kwa sasa serikali inaandaa mpango ya kuboresha sekta hiyo kwa njia ya kilimo cha umwagiliaji na utumiaji wa mbolea ili kuleta tija zaidi.
"Katika sekta ya kilimo, bado tunazidi kujitangaza ili kuzidi kuwavutia wawezekaji, kwani sekta hii ndio kitega uchumi cha Watanzania wengi na tegemeo kubwa kwa taifa letu", alisema Kikwete.
Alisema, kwa sasa kilimo cha umwagiliaji ndicho kinachopewa kipaumbele, ambapo aliwataka wawekezaji wa sekta ya kilimo kuja nchini kwa ajili ya kuwekeza hasa ikizingatiwa kwamba Tanzania ina vyanzo vingi vya maji kama mabwawa, mito, mifereji ambayo inafaa kwa kilimo cha umwagiliaji.
mwisho.

No comments: