Friday, March 16, 2007

WANANCHI NA UCHUMI WA tANZANIA


Mara nyingi hotuba za viongozi wakuu wa serikali za awamu ya tatu na ya nne wamekuwa wakizungumzia juu ya kuimarika kwa uchumi baada ya marekebisho mbalimbali ya sera za uchumi. Benki Kuu ya Tanzania huwa inazungumzia mambo ya mfumuko ya bei, viwango vya ubadilishaji wa fedha za kigeni na riba za mabenki na taasisi za fedha ili kuelewa tumetoka wapi katika safari ya kuimarisha uchumi. Ni muhimu kuangalia hali ya uchumi wa miaka kumi na tano iliyopita katika miaka ya mwazo ya miaka ya 1990. Kati ya mwaka 1990 hadi 1995 mfumuko wa bei yaani ongezeko la bidhaa zote za mlaji zilikuwa zinaaongezeka kwa kati ya asilimia 30 hadi asilimia 36 kila mwaka. Kwa hali hiyo fedha ilipoteza thamani kwa sababu uwezo wake wa kununua bidhaa ulipunguka sana. Wakati huo vile vile ilibidi riba zinazotozwa na kutolewa na mabenki kwa amana ilibidi ziongezeke kwa sababu ya kuteremka kwa bei. Benki ingepata hasara kama ingekopesha fedha kwa riba ya asilimia kumi wakati mfumuko wa bei ulikuwa asilimia thelathini vile vile wakaweka fedha zao katika mabenki ilibidi walipwe riba za amana za juu ingawa hii haikuwezekana kwa sababu benki zilikuwa mbili NBC na CRDB zilikuwa na ukiritimba wa shughuli za benki na wawekezaji amana hawakuwa na uchaguzi wa wapi waweke amana zao ili wapate riba ya juu zaidi . Serikali ya awamu ya tatu ilijitahidi kukusanya kodi za mapato, ushuru wa forodha na kodi ya ongezeko la thamani mwaka 1995 mamlaka ya kodi TRA ilikuwa inakusanya Tshs 30 bilioni kwa mwezi lakini baada ya kuongeza bidiii ya kusimamia makusanyo ya kodi alipofika mwaka 2000 makusanyo ya kodi kwa mwezi yalifika Tshs 156 bilioni na hii imeongezeka hadi zaidi ya Tshs 260 bilioni kwa mwezi katika awamu ya nne. Kuongezeka kwa makusanyo ya kodi kulikuwa na faida mbili muhimu. Serikali iliweza kupunguza nakisi ya bajeti ya serekali na hivyo kupunguza kiwango cha fedha ambazo serikali hukopa kutoka kwa mabenki na hasa Benki Kuu. Ukopaji huu wa serikali ukiwa wa kiwango cha juu sana huchangia mfumko wa bei kwa ajili ya kuongezeka kwa mzunguko wa fedha wakati uzalishaji wa bidhaa huwa haungezeki. Mapato ya ndani ya serikali yakiongezeka ukopaji kutoka nchi za nje hupungua la muhimu zaidi ni kwamba uwezo wa kulipa madeni ya wafadhili huongezeka na matokeo yake ni kupata misamaha ya madeni kwa nchi maskini kama Tanzania katika mpango wa HIPC na nchi inakuwa inaaminika na wafadhili kwa kuwa inaonekana inaweza kukopesheka. Serikali iliongeza nidhamu katika matumizi ya fedha za serikali na kupunguza ujazi au ongezeko la fedha kutoka Benki Kuu `money supply` kufuatana na sera ya fedha ya kubana ongezeko la fedha katika uchumi kufikia asilimia 10 - 12 kwa mwaka. Kwa kutumia mikakati kama kuuza dhamana za serikali fedha za ziada katika uchumi (excess liqudity) hupungua na hiki ndicho kinachosaidia kupunguza mfumuko wa bei. Mwaka 1995 mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 30 lakini kufikia mwaka 2002 mfumuko wa bei ulipungua hadi kufika asilimia tano na hadi sasa mfumko wa bei umefikia asilimia 4.4. Hii ina maana bila kuongeza mishahara au mapato mengine kwa wananchi kwa fedha zile zile kwa mwezi kama mapato kushuka kwa mfumko wa bei kunawawezesha walaji kununua bidhaa nyingi zaidi. Bidhaa hizi ni pamoja na vyakula, nguo, viatu na bidhaa za ngozi, gharama za usafiri, bidhaa za ndani kama radio na TV, gharama za burudani na kwa ujumla bidhaa zote za mlaji. Wananchi na kawaida hufaidika na kushuka kwa mfumuko wa bei kwa sababu matumizi ya mwananchi wa kawaida kwa chakula ni zaidi ya asilimia 64% ya mshahara au mapato kwa mwezi ya mwananchi. Kuimarika kwa uchumi mkuu au `macro-economic stability` ni pamoja na ongezeko dogo la bei za bidhaa zote kwa jumla, ubadilishaji wa fedha za kigeni usiobadilika mara kwa mara na vile vile riba za mabenki zinatabirika. Wataalam wa uchumi wanasema kwamba kudhibiti mfumuko wa bei huvutia wawekezaji wa nje na ndani ya nchi kwa sababu inakuwa rahisi zaidi kwa wawekezaji kupanga mpango yao ya biashara. Hii ni pamoja na kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji kama kuwa na vivutio vya misamaha ya baadhi ya kodi kwa wawekezaji, uboreshaji wa miundo mbinu, utawala bora na kupiga vita rushwa . Kati ya mwaka 1995 uwekezaji kutoka nje umeongezeka kutoka dola za kimarekani milioni kumi kwa mwaka hadi kufikia dola 350 mnamo mwaka 2004 na juhudi zikifanywa kuvutia uwekezaji kuna uwezo wa kuongezeka kwa uwekezaji hadi kufikia dola 500 milioni kwa mwaka katika kipindi kifupi kijacho na haya yamewezekana kwa kuimarisha uchumi mkuu na hasa kuthibiti mfumuko wa bei. Matokeo ya ongezeko la uwekezaji ni pamoja na kuongeza bidhaa zinazozalishwa soko la ndani kwa bei nafuu na ukuzaji wa ajira na fursa nyingi za kuongeza mapato kwa waajiriwa na wale wanaotoa bidhaa huduma kwa wawekezaji kama sekta ya viwanda na madini. Wakulima wa pamba wanapata soko la ndani kama viwanda vingi vya nguo vikianzishwa. Hivi ni kweli kwa malighafi zote zinazozalishwa katika sekta ya kilimo na kufugwa kwa viwanda vipya vinavyoanzishwa. Lakini watanzania hawategemewi kula uchumi mkuu ulioimarika au `macro-economic Stability. Kuimarika kwa uchumi ni lazima kusaidie ukuaji wa sekta mbalimbali za uchumi na shughuli za kibiashara, viwanda na uzalishaji kwa wawekezaji au micro-economic units.Ukuaji wa uchumi ukawa chini ya . asilimia 4.4 mwaka 1995 na sekta nyingine zikawa hazikui kabisa hasa viwanda ambavyo vilidumazwa na sera mbalimbali ikiwepo kulengeza masharti ya biashara ambapo bidhaa nyingi ziliangizwa kutoka nje ya nchi kwa bei nafuu na hivyo bidhaa za ndani kukosa soko. Kuwa na sera nzuri za biashara, viwanda, madini na utalii kumeongeza uzalishaji katika sekta hizi. sekta ya madini sasa inakuwa kwa asilimia 17 na kuchangia asilimia nne katika pato la Taifa. Sekta ya viwanda inakua kwa asilimia 8.4 na kuchangia asilimia katika pato la taifa. Vilevile sekta ya utalii imekuwa ukifanya vizuri kwa ukuaji wa asilimia 12 na kuchangia asilimia 16 katika pato la taifa na kupata shilingi bilioni 600 fedha za kigeni ikiwa nyuma ya kilimo na madini katika kukuza akiba ya fedha za kigeni. Ili wananchi wanufaike kwa ukuaji wa uchumi kuna umuhimu katika maisha yao kuwa bora zaidi kwa kupunguza umaskini. Ndiyo maana serikali ikabuni MKUKUTA kama sera ya ukuaji uchumi na upunguzaji umaskini. Bajeti kubwa ya serikali inaelekezwa katika sekta za elimu, afya, barabara za vijijini na mapambano zidi ya HIV-Aids, Malaria, TB na magonjwa mengine. Kuimarika kwa uchumi ni lazima kuwezeshe wananchi wengi zaidi kupata huduma za jamii na za kiuchumi. Tanzania ni nchi maskani ambayo asilimia hamsini ya watu wake huushi kwa matumizi ya chini ya dola moja ya kimarekani kwa siku. Hivyo sera ya uwezeshaji, na sera ya kurasimisha mali na biashara katika sekta isiyo rasmi ina lengo la kuongeza ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini. Watalaam wa uchumi wa mashirika ya kimataifa ya fedha na wa hapa nchini wanaamini kuwa kama uchumi ikikua kwa asilimia 8 hadi 10 lengo la kupunguza umaskini litafikiwa. Tanzania ni moja wapo ya nchi ambazo zilitia saini mwaka 1999 kufikia malengo ya milenia (millenum Development Goals) Kuna kila dalili kwa Tanzania itafika baadhi ya malengo hayo ifikapo mwaka 2015 kama uchumi utaendelea kuimarika. Malengo hayo ni kupunguza umaskini wa kipato kwa nusu ifikapo mwaka 2015. Lengo jingine ni kila mtoto anayefika umri wa kwenda shule aingie shule za msingi au (Universal Primary Education) na lengo hili limefikiwa zaidi ya asilimia 90. Malengo mengine ni kupambana na maradhi kama VVU?Ukimwi, TB na Malaria. Kupunguza umaskini ni pamoja na kuondoa njaa na kuongezeka kwa lishe kwa watu walio wengi nchini. Melengo mengine ya milenia ni pamoja na kupunguza vifo vya kina mama wazazi, na vifo vya watoto chini ya miaka mitano malengo mengine ni kuwawezesha akina mama kiuchumi na kuboresha mazingira kwa kuwa na maendeleo endelevu au environmental sustainability` lengo lingine ni kukuza ushirikiano na mataifa mengine katika maendeleo. Kukua kwa uchumi ni lazima kuendane na kupunguza tofauti kati ya wananchi wenye vipato vya juu na wale wenye kipato cha chini. sera za MKURABITA, MKUKUTA vitaweza Tanzania ukuze uchumi na kuongeza fursa za uchumi kwa watu wake wengi au wanavyosema watalaam ?economic groth with social justice. Ukuaji wa uchumi ni lazima ulete maendeleo ya kiuchumi na huduma za jamii kwa sababu kama Mwalimu J. Nyerere alivyokuwa akasema maendeleo ni lazima yaboreshe maisha ya watu. Hivyo ukuaji wa uchumi ni lazima ulete maisha bora kwa Watanzania wote ambalo ni lengo kuu la awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.

No comments: