Friday, May 11, 2007

Na Aisha Mbaga


UCHUMI wa MALAWI

UCHUMI-MALAWI:Kuwa ''Mwanafunzi Bora'' Kunaweza Kuwa Kubaya Kwako Pilirani Semu-Banda BLANTYRE, Aprili 17 (IPS) - Miaka mitano baada ya njaa ambapo zaidi ya watu 1,000 nchini Malawi walifariki dunia na wengine milioni 8 kati ya milioni 12 nchini humo walikabiliwa na njaa, kumbukumbu inayouma ya ushauri wa sera mbovu bado inaendelea. Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) na Benki ya Dunia zililaumiwa kutokana na janga hilo ambalo liliipiga Malawi wakati wa njaa ya mwaka 2002. Shirika la kimataifa la kupigania haki za binadamu la Action Aid, kwa mfano, lilionyesha katika taarifa ya mwezi Oktoba 2002 kwamba IMF imeitaka serikali ya Malawi kuuza akiba ya nafaka kulipia deni lililokopwa na chombo kilichosajiliwa kisheria cha Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA). Ripoti hiyo iliyojulikana kama, ‘‘State of disaster: Causes, consequences and policy lessons from Malawi'', pia ilitaja Benki ya Dunia. Action Aid iliilaumu Benki ya Dunia kutokana na ‘‘kushinikiza'' Malawi kuuza mahindi kwa Kenya kulipia deni ambalo nchi hiyo ilikuwa ikidaiwa na Benki hiyo. Halafu Waziri Bakili Muluzi pia alitangaza wazi wazi kwamba Benki hiyo imekuwa ikishawishi serikali kuhifadhi fedha za kigeni kuliko nafaka. Nafaka, Benki hiyo ilisema, zinaweza kupoteza thamani. Hata hivyo, IMF na Benki ya Dunia zilikanusha shutuma hizo kwa kusema kwamba ‘‘zilikuwa washauri tu'' kwa serikali juu ya hifadhi yake ya nafaka. Walisema kwamba sababu za uhaba wa chakula nchini Malawi zilikuwa ngumu ikiwa ni pamoja na serikali kukaa kimya kutoa onyo la haraka, kupotosha habari katika masoko ya ndani na usimamiaji mbovu wa hifadhi ya chakula. Kufuatia shutuma hizo na kujibu shutuma hizo, mahusiano kati ya mashirika ya wafadhili na serikali yaliathirika. Hii ilisababisha kuchelewa kwa wafadhili kuchukua hatua wakati wa mgogoro wa chakula. Malawi imekuwa ikitegemea zaidi wafadhili kwa miongo minne. Fedha za wafadhili ambazo imeshazipata zinakaribia asilimia 40 ya bajeti ya taifa. Nchi hiyo imeshindwa kung’ata mkono ambao unailisha. Hivyo, pamoja na madai hayo ya sababu za mgogoro wa chakula, serikali ilikamilisha mageuzi ya kiuchumi katika kuzingatia masharti yaliyowekwa na Benki hiyo na IMF. Ikiwa kama zawadi, taasisi hizo zilifutia Malawi madeni yake mengi ya nje yanayofikia dola bilioni 2.97 Septemba 2006. Kumbukumbu za njaa hiyo na sababu yake bado zinaendelea kuwepo. Baadhi ya Wamalawi wanataka nchi hiyo kujinasua kutoka kwenye mtego wa taasisi hizo. Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Maendeleo ya Jamii ya Umoja wa Mataifa, Thandika Mkandawire, ambaye yeye mwenyewe ni raia wa Malawi, ni mmoja wa watu ambao anahofia mahusiano ya nchi hiyo na nchi wafadhili na taasisi za fedha za kimataifa. Anasema pamoja na Malawi kubatizwa jina la ‘‘mwanafunzi bora'' wa Benki hiyo na IMF kati ya mwaka 1980 na 1990, nchi hiyo inasimama kama mshtaka wa mahusiano ya misaada katika miongo mitatu iliyopita. Kati ya mwaka 1979 na 1999 Malawi ilichukua nafasi miongoni mwa kile IMF ilikipatia sifa ya ‘‘mtumiaji wa muda mrefu mno'' wa vifaa vyake. Taifa hilo lilikuwa na programu sita na IMF. Miaka 17 kati ya miaka 20 Malawi ilikuwa chini ya programu moja ya IMF hadi nyingine. ‘‘Katika nyaraka za IMF na Benki ya Dunia zilizokuwa zikifanyia tathmini matokeo ya sera za uchumi wa Afrika kati ya mwaka 1981 na 1998, Malawi iko juu zaidi katika orodha ya ‘warekebishaji bora' huku ikiwa imejitokeza mara saba, ikifuatiwa na Uganda na Kenya zikiwa za tano,'' anasema Mkandawire. Pamoja na ‘‘sifa hizo'', pato la taifa la Malawi lilishuka kutoka dola za Kimarekani 156 mwaka 1980 hadi dola 143 mwaka 1990. Hata ilipofika mwaka 2003 Malawi ilikuwa bado haijafikia kiwango cha pato la taifa cha mwaka 1979, kulingana na takwimu za Benki ya Dunia. Ripoti ya umaskini na kukosekana kwa utulivu iliyotolewa mwaka jana na serikali na Benki ya Dunia inaonyesha kwamba kumekuwepo na mafanikio madogo mno katika kupunguza umaskini na kukosekana kwa usawa. Mchanganyiko wa ushauri mbovu wa kisera na utawala wa kimabavu umezalisha miongo miwili iliyopotea kwa Malawi, anasema Mkandawire. Hakupendezewa na kukubali makosa kwa taasisi hizo au Mikakati ya Benki hiyo ya Kupunguza Umaskini. Ushauri wao umesababisha kuanguka kwa uwekezaji wa umma katika mtaji wa kimaumbile na kibinadamu, anasema. ‘‘Jambo ambalo hawaonekani kulitambua ni kwamba ongezeko la makosa limesababisha uchumi ambao haujarekebishwa vizuri na kushikiliwa katika mtego wa ukuaji mdogo,'' anasema Mkandawire. Mkandawire ana wasiwasi zaidi na jinsi ya kuingiliwa na nguvu za nje kunavyosababisha mataifa ya Afrika kupoteza uhuru wake. Mwaka 2002 IMF ilisitisha misaada yake ya kiuchumi kutokana na kile ambacho imekiita usimamizi mbovu wa uchumi chini ya rais wa zamani Muluzi. IMF ilirejesha programu yake baada ya utawala wa Bingu wa Mutharika, ambaye aliingia madarakani Mei mwaka 2004, kukubali kutekeleza sera zinazosimamiwa. Kwa njia hii rikodi zinazoeleweka za kutekeleza sera ziliundwa ili kuwarejesha wafadhili. Utekelezaji wa sera kwa mwaka wa kwanza ulishuhudia IMF na Benki kuizawadia Malawi kufuta asilimia 90 ya madeni yake ya kigeni. Msamaha wa madeni ulitafsiriwa kwamba Malawi ingeokoa dola za Kimarekani milioni 100 kama akiba ya kununulia bidhaa zake kutoka nje kwa mwaka kwani nchi hiyo iliendelea kuwa na mtaji ambao ungetakiwa kutumika katika kulipia madeni. Mkuu wa sera katika Action Aid Malawi, Collins Magalasi, pia hajaridhishwa na tabia ya mashirika wahisani. Anatoa mwito kwa nchi mfadhili wakuu wa Malawi, serikali ya Uingereza, kuongeza msaada wake wa kifedha ambao katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ulifikia wastani wa pauni milioni 54.1 kwa mwaka, ambapo ni asilimia 0.0009253 tu ya pato la ndani la mwaka la Uingereza. Magalasi analaumu kuwa Wamalawi 70,000 wanafariki dunia kila mwaka kutokana na magonjwa yasiyozuilika. Kipato cha watu wote kikichanganywa hakilingani na ruzuku za kilimo ambayo Umoja wa Ulaya unatumia kwa wakulima wake. Wakati akielezea kuridhishwa kwake na misaada ya wafadhili ambayo nchi hiyo inapokea, Mutharika ametoa pia mwito wa ‘‘sera zinazobuniwa ndani ambazo zinapaswa kuungwa mkono na washirika wengine''. Katika mwaka wa fedha 2005/2006 serikali ilianza kutekeleza sera iliyoandaliwa ndani ya nchi iliyojulikana kama Mkakati wa Kukuza Uchumi na Maendeleo wa Malawi (MGDS), ambao utaendeshwa kwa kipindi cha miaka mitano. Mutharika anaona mkakati huo mpya kama chombo cha kuhamisha vipaumbele kwani ulibuniwa na Wamalawi. Wakati huo huo, unafanya kazi ya kurejesha nidhamu katika masuala ya fedha. Wafadhili wameunga mkono sera hiyo, kwa kukubali kuruhusu nafasi kwa sera zinazobuniwa na Wamalawi; na watu wa kawaida badala ya zile zinazobuniwa na wanauchumi na kuzimiliki. Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Haki ya Uchumi wa Malawi (Mejn), Andrew Kumbatira, anakubaliana kwamba MGDS ni sera iliyobuniwa ndani ya nchi ambapo mawazo ya ndani yamepewa nafasi kubwa mno. Anakubali kwamba ‘‘kuna sera zinazofanana na hizo katika mataifa mengine yanayoendela. Hii inaonyesha kwamba sera bado inaongozwa na wafadhili. Lakini jambo zuri kuhusu sera hii mpya ni kwamba mikutano ya ndani ya mashauriano ilikuwa mingi''. (END/2007)

No comments: