Thursday, March 29, 2007

Usultani Hadi Taifa Huru

Manispaa ya Zanzibar imegawanyika kihistoria katika maeneo mawili, nayo ni Mji Mkongwe na

Ng’ambo. Kuibuka na kukua kwa maeneo haya tangu karne ya 19, kumekuwa katika misingi ya

kiuchumi. Mji Mkongwe uliojengeka vema, ulikuwa kwa ajili ya matajiri na wasomi wakati viunga vya

Ng’ambo, vikawa kwa ajili ya walalahoi.

Mji Mkongwe ulianza kukua taratibu, awali kama makazi ya wavuvi kwenye Rasi ya Shangani katika

karne ya 12. Ulikuwa mji wa Kiswahili hasa, baadhi ya watu wakijishughulisha na sanaa za mikono, na

ikawa sehemu ya biashara zile ndefu zilizofanywa kwa njia ya bahari.

Kunako karne ya 17, Malkia Fatima alipotawala Unguja ya Kati, Mji wa Zanzibar uligeuka na kuwa

makao makuu ya falme yake. Alirithiwa na mwanawe Hasan, anayesemekana alifanya mengi katika

ujenzi wa Mji Mkongwe. Kuingia kwa wafanyabiashara wa Kireno pamoja na wale wa Kiarabu mwaka

1822, kulisababisha Waswahili kuhamia pande za mashariki mwa Mji Mkongwe.

Utawala wa Wareno ulipoanza kusambaratika katika Afrika Mashariki, Waarabu wa Oman, ambao awali

walikuja kama wafanyabiashara, walitwaa madaraka kisiwani Zanzibar. Waligeuza uchumi wa Zanzibar

kutegemea zaidi kilimo cha mashamba makubwa, ndipo uzalishaji wa karafuu ukashamiri na kukipatia

kisiwa umaarufu mkubwa. Japokuwa wamiliki ardhi hiyo walijenga nyumba mashambani, watu wengi

walipendelea zaidi makasri kandokando ya bahari, karibu na hekalu la Sultani.

Eneo ulipokuwa mji wa Zanzibar, lilikuwa jambo la umuhimu mkubwa, hasa wakati Sultani wa Oman,

Seyyid Said alipokuja Zanzibar na akaamua kuufanya kuwa makao makuu. Iliripotiwa kwamba idadi ya

watu kwenye mji huo ilikuwa kati ya 10,000 na 12,000.

Ujio wa Sultani Seyyid Said, ulileta zama mpya kwani mji huo uligeuka kuwa kituo kikuu cha biashara

katika Pwani ya Mashariki mwa Afrika. Misafara ya kibiashara ilistawi kwa kiasi kikubwa na yenye faida

pia, ikihusisha uuzaji watumwa kutoka pwani hii. Watumwa hao walitumiwa kuzalisha bidhaa

mbalimbali pamoja na dhahabu. Biashara ilistawi na misururu kutoka bara, ilileta pembe za ndovu,

dhahabu na watumwa ambao walifanya kazi kwenye mashamba hayo makubwa.

Ni mtawala huyo huyo ambaye aliweka misingi ya kuendeleza mji huu na pia, licha ya karafuu, mazao

mengine yaliyozalishwa kwa kiasi kikubwa ni minazi. Uzalishaji wa mazao haya ya biashara, ulisaidia

kukuza biashara, ikizingatiwa zaidi kwamba mji huu ulijaliwa kwa asili kuwa na bandari nzuri zaidi

kisiwani. Bandari iligeuka kuwa kituo kikuu cha usambazaji na pia kutoa mwelekeo kamili wa hali ya

biashara katika eneo hili.

Kwa vile mazingira yalikuwa mazuri kwa ajili ya shughuli za kibiashara, watu kutoka mashambani

walihamia mijini, wakisaka nafasi nzuri zaidi za ajira. Kwa misingi hiyo, ardhi ilihitajika kwa kiasi

kikubwa kwa sababu za kibiashara. Zama hizi, Waarabu, Wahindi na Wapersia, walidhibiti umiliki wa

ardhi kiasi cha kulazimisha wenyeji kununua ardhi kutoka kwa wamiliki wake kwa bei kubwa.

Kwa vile wakati huo hapakuwepo mipango mahususi ya kulinda na kudhibiti maendeleo ya makazi

mapya, ilifika hatua watu wakabuni makazi yasiyo na ramani kwenye eneo la Ng’ambo, jambo

lililosababisha makazi kuwa katika hali ya chini, kukosekana huduma za kijamii na miundombinu

muhimu.

Mwaka 1890, Zanzibar iliwekwa chini ya uangalizi wa Uingereza, Sultani akiwa bado na madaraka

makubwa ya kisiasa hata hivyo. Ni wakati huu ambapo, mipango mbalimbali ilianzishwa na chini ya

mpango huu, Waarabu waliendeleza maeneo ya Kidongo Chekundu, Sebleni, Kwahani na kadhalika.

Kabla ya uhuru, vyama kadhaa vya siasa tayari vilikuwa vikifanya kazi. Vyama vikuu vilikuwa Zanzibar

National Party (ZNP), kilitawaliwa zaidi na wasomi ambao ni wachumi. Chama kingine kilikuwa Afro

Shiraz (ASP), chama kilichokuwa na Waafrika wengi zaidi na kikiwa na mshikamano mkubwa wa

makundi ya wanyonge.

Katika uchaguzi wa mwisho kabla ya uhuru Julai mwaka 1963, ZNP kilichoshirikiana na chama kingine

kidogo cha Pemba, kilifanikiwa kupata wingi wa kura katika baraza jipya la kutunga sheria na Desemba

1963, Zanzibar ilikuwa huru kutoka kwa Waingereza. Mwezi mmoja baadaye, Januari 12 mwaka 1964,

serikali mpya ya Sultani iliangushwa baada ya kufanyika mapinduzi visiwani.

Sultani mwenyewe aliikimbia Zanzibar na ASP ikaingia madarakani na kuitawala nchi hadi mwaka 1977,

kilipoungana na wenzao wa Tanzania Bara, TANU na kuunda Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho

hadi leo kipo madarakani. Licha ya kuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zanzibar

imekuwa na mamlaka makubwa ya kiserikali kujitawala, isipokuwa kwa masuala ya muungano. Masuala

hayo ya muungano ni kama vile ulinzi, sera za kigeni na mambo ya ndani. Zaidi ya hapo, Zanzibar inalo

Bunge lake, likijulikana zaidi kama Baraza la Wawakilishi lakini pia, inawakilishwa katika Bunge la Jamhuri

ya Muungano wa Tanzania, ikiwa na wabunge 50 huko.

Mwaka 1995, muswada ulipitishwa na kuwa sheria iliyoanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa na

katika uchaguzi wa kwanza, CCM ilishinda kama ilivyokuwa tena mwaka 2000 na uchaguzi wa tatu chini

ya mfumo huo utafanyika mwaka 2005.

Manispaa ya Zanzibar iko ndani ya eneo la Mjini Magharibi ambalo limegawanywa katika wilaya kuu

mbili; Wilaya ya Mjini na Wilaya ya Magharibi, kila moja ikiwa na mkuu wa wilaya aliyeteuliwa na rais.

Mipaka ya kiutawala kwa manispaa hii ni kama ile ya Wilaya ya Mjini. Hata hivyo, kwa mujibu wa

michoro iliyotokana na mipango ya mwaka 1982, Mji unachukua eneo kubwa zaidi ya mipaka ya

Manispaa na sehemu yake iko Wilaya ya Magharibi.

Halmashauri ya Manispaa pia, huendesha shughuli zake kwenye maeneo hayo ya Wilaya ya Magharibi,

ambayo kimsingi, yako nje ya mipaka ya awali (lakini ndani ya mipaka iliyowekwa kwa mipango ya Mji).

Mipaka hiyo mipya bado haijaidhinishwa na Wizara ya Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa kuwa ndiyo

mipaka rasmi ya manispaa.

Hali hii ya utata wa mipaka ya zamani na mipya, inasababisha mgongano kati ya taasisi na vikundi

nyingi. Kwa mfano, madiwani wa Wilaya ya Magharibi, hawapo kwenye Halmashauri ya Manispaa ya

Zanzibar (ZMC), japokuwa ZMC yenyewe inaendesha shughuli zake. Kwa vile mji umekua na kupanuka

zaidi ya manispaa, inaelekea haitachukua muda, mipaka ya manispaa yenyewe itabadilishwa. Kwa msingi

huo, ripoti hii kwa hiyo, inafuata mipaka mipya iliyopendekezwa na Tume ya Ardhi na Mazingira

(COLE) katika mpango ule wa mwaka 1982

Japokuwa idadi ya kata kwenye Wilaya ya Magharibi ni 10, tatu tu ndizo ziko ndani ya mipaka hii

mipya. Wilaya ya Mjini ina majimbo 13 wakati Wilaya ya Magharibi inazo tatu katika mipaka hiyo mipya.

Kila jimbo huwakilishwa na mbunge na mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwenye vyombo hivyo vya

kutunga sheria Zanzibar na katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuna jumla ya kata 26 wilayani

Mjini Magharibi na tatu kwenye Wilaya ya Magharibi.

Kata hizo huwakilishwa kwenye Halmashauri ya Manispaa na madiwani wanaochaguliwa. Kwa sasa,

madiwani kutoka Wilaya ya Mjini ndio wanawawakilisha wananchi kwenye Baraza la Manispaa ya

Zanzibar.

Meya huchaguliwa kutoka miongoni mwa madiwani. Kata zimegawanywa tena katika shehia na kila

shehia ina kiongozi anayeitwa sheha. Wilaya ya Mjini ina shehia 39 wakati Wilaya ya Magharibi ina

shehia 23, sita zikiwa ndani ya mipango mipya ya mipaka. Japokuwa bado haijachapishwa kwenye

gazeti la serikali, kuna shehia mpya ya Karakana iliyoko Chumbuni, na hii inafanya jumla ya shehia kuwa

40

Zanzibar, ikijulikana zaidi kama visiwa vya marashi ya karafuu kutokana na sifa ya uzalishaji zao hilo,

inajumuisha visiwa viwili vikubwa ambavyo ni Unguja na Pemba. Manispaa ya Zanzibar iko katikati ya

Pwani ya Magharibi ya Kisiwa cha Unguja. Eneo hili lina ubapa kiasi, huku kukiwa na mwinuko kwa

upande wa magharibi, na kutoka Pwani, kuna mwinuko kidogo, kuelekea mashariki.

Kwa wastani, Pwani yenyewe iko meta 6.6 juu ya usawa wa bahari na eneo lililo lililoko chini zaidi ni

Tomondo, ambako kuna bonde lenye kina cha kati ya meta 10 hadi 15 chini ya usawa wa bahari

Eneo lililo juu zaidi ni tuta la Masingini, meta 100 kwa upande wa mashariki wakati kwa upande wa

magharibi, kuna visiwa vinne ambavyo ni Chapwani, Changuu, Kibandiko na visiwa vya Bawe (tazama

ramani 1.1):

Zanzibar iko kwenye ukanda wa kitropiki na mvua hutegemea kwa kiasi kikubwa majira na mabadiliko

ya pepo za Bahari ya Hindi. Masika ya Zanzibar huzalisha asilimia 40 ya mvua ya mwaka mzima na

huanza Machi hadi Mei. Kipindi cha ukavu, lakini chenye ubaridi kiasi kiitwacho Kusi, huanzia Juni na

kumalizika Septemba wakati Vuli yenye asilimia 20 ya mvua za mwaka mzima, huanzia Oktoba na

kumalizika Desemba. Kipindi cha pepo zitokazo kaskazini kwenda mashariki (Kaskazi), huanza Januari

na kumalizika Machi. mji huu hupata milimita 1,500 hadi 2,000 za mvua kwa mwaka.

Manispaa ya Zanzibar ndio makao makuu ya visiwa hivi na ndio kitovu chake kiuchumi, kisiasa na hata

kitamaduni. Hapa ndio makao makuu ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Huchangia kwa kiasi kikubwa

katika suala zima la biashara na utalii, sekta zinazochangia zaidi mapato ya fedha za kigeni.

Waweza kufika kwenye kisiwa hiki kupitia bandari au uwanja wa ndege wa kimataifa. Ni katika

manispaa hii ya Zanzibar pia, kuna sehemu muhimu kama vile ofisi za Serikali, sehemu za ibada,

biashara na zile za starehe na mapumziko.

Mpangilio wa makazi mjini hapa upo katika aina tano, na umetokana na mipango na taratibu tofauti

zilizoandaliwa (tazama ramani 1.2):

Mji Mkongwe uko upande wa magharibi wa barabara kuu. Ukiwa ndio bandari kongwe, inayotambulika

siku nyingi kihistoria, ina maeneo na majengo yaliyosanifiwa kwa aina yake na ni urithi wa kitamaduni

kwa Wazanzibari na pia ni kivutio kikubwa kabisa cha watalii.

N’gambo ni maeneo mengine makongwe, lakini ambayo hayajachorewa ramani. Yapo upande wa

mashariki wa barabara hiyo na yaliendelezwa kati ya mwaka 1840-1923. Maeneo yenyewe ni

Mwembetanga, Vikokotoni and Kiswandui.

Yapo maeneo mengine ya Ng’ambo yaliyofanyiwa michoro kiasi, kulingana na mipango na taratibu za

mwaka 1958. Maeneo haya ni pamoja na Kidongo Chekundu, Kwahani na Jang’ombe.

Maeneo mapya ambayo bado hayajapimwa, yaliendelezwa mara baada ya kuanzishwa kwa sera za

biashara huria. Haya ni pamoja na Chumbuni, Munduli, Darajabovu, Tomondo, Uholanzi na Kitosani.

Yapo maeneo mapya yaliyopimwa tayari. Maeneo haya yaliendelezwa baada ya michoro iliyoandaliwa

mwaka 1982 na maeneo yenyewe ni Mwanakwerekwe, Mombasa, Mpendae na Chukwani.


mwisho

No comments: